Udhaifu Wa JK; Tafsiri Yangu


“
 OUR President is important; but, he is not Tanzania. All of our people 
organaized together are Tanzania”- (Julius Nyerere, Julai  29, 1985)
Ndugu zangu, 
Watanzania wengi hatuna mazoea ya kusoma, hata makala za magazetini ukiachilia mbali vitabu vya taarifa na hadithi. Ndio, tu wavivu wa kusoma.
Kigong’onda ni aina ya ndege.  Ndege huyu  ana mdomo mrefu na anapenda sana kugongagonga mti kwa mdomo wake. Ndivyo anavyojipatia ridhiki yake. 
Lakini,
 kwa hulka yake ya kugong’onda kila kilicho mbele yake, basi, hata 
ukimwekea mti wa chuma porini, kigong’onda atahangaika nao mpaka damu 
zimtoke mdomoni. Ni hulka yake.  Kiongozi hapaswi kuwa kama kigong’onda. 
Kuna hoja mezani juu ya udhaifu wa JK, imetokea Bungeni.  Yumkini,
 kama mwanadamu, JK ana mapungufu na udhaifu wake, nani asiye na 
mapungufu na udhaifu? Lakini, tukimzungumzia JK kama taasisi ya ’ 
Urais’, namwona Rais anayejipambanua na waliomtangulia. Ni  kwa 
kujitahidi kufanya yale yalo nafuu na yenye manufaa kwa nchi yetu  kwenye mfumo dhaifu uliopo.  
 Wanadamu
 tunapaswa kuhukumu dhamira ya mtu na si matokeo. Bado namwona JK kama 
kiongozi mwenye dhamira njema kwa nchi yetu. Nauona ujasiri ndani ya JK.
 Ni ujasiri wa kufanya yale ambayo, hata ndani ya chama chake 
hayakuwezekana kufanywa na Mwenyekiti wa chama huko nyuma. Na bila 
shaka, kuna wahafidhina ndani ya chama chake wanaomwona JK kuwa ni 
dhaifu kwa mantiki hiyo. Kuna wanaoamini, ndani ya CCM, kuwa Rais wa 
chama tawala anayekaa na kuongea na wapinzani Ikulu ni Rais dhaifu!
Na
 hata haya tunayoyashuhudia sasa, yumkini ni matokeo ya dhamira njema ya
 JK. Naamini, kwa tunavyoenenda sasa, Tanzania atakayoiacha  JK
 haiwezi tena kurudi kuwa kama ilivyokuwa kwa Julius Nyerere, Ali Hassan
 Mwinyi na Benjamin Mkapa. JK amepanua uhuru wa Watanzania kuchangia 
fikra zao bila hofu. Siku zote, hofu haijengi nchi.
Maana,
 tumefika hapa kutokana na mfumo dhaifu unaozaa Serikali dhaifu, unaozaa
 Bunge dhaifu na unaopelekea pia kuzaa vyama dhaifu vya siasa ikiwamo 
chama tawala. Na chimbuko lake ni Katiba ya Nchi iliyo DHAIFU. Ndio, 
tatizo la nchi yetu ni tatizo la kimfumo. 
Ni tatizo lililoasisiwa tangu Awamu ya kwanza ya Urais.  Angalia, Katiba yetu inampa nguvu nyingi sana Rais. Tuna bahati tu hajatokea Rais anayeamua kuzitumia ipasavyo nguvu hizo.
Nimeona katuni ya ndugu yangu Masoud Kipanya kwenye gazeti la Mwananchi la jana, Juni 23, 2012.  Kipanya alionyesha foleni ndefu ya wapiga kura Watanzania walio tayari kumpigia kura Rais Dikteta.   
Niliogopeshwa na michango ya  maoni
 ya Watanzania juu ya katuni ile. Wengi walionekana kuikubali hali hiyo.
 Kuwa kwao kwa hali ilivyo sasa ni heri kutawaliwa na dikteta kuliko 
Rais dhaifu!
Inasikitisha na inaogopesha kuona kuwa tumefika hapa. Naamini mimi na wengine wengi tuliokulia enzi za chama kimoja  na
 Rais mmoja ambaye ni kila kitu, tusingependa kurudi huko tulikotoka. 
Nikayasoma jukwaa moja maoni ya Mtanzania Ludovic Mwijage aliyejaribu 
kuonyesha ubaya wa udikteta. Hapo chini nimeweka kitabu cha Mwijage 
kilicho kwenye maktaba yangu. Kwa mimi niliyesoma kitabu chake, 
ningeshangaa kama Mwijage angeunga mkono hoja ya kumwona JK dhaifu na 
kutamani Rais Dikteta.
Ukweli,
 sisi wa ’ Kizazi Cha Azimio’ tuliwaona wazazi wetu wakiishi katika hali
 ya hofu na mashaka. Waliishia kunong’ona tu pale walipotaka kuishutumu 
Serikali na Rais aliye madarakani. 
Mjumbe wa nyumba kumi alikuwa ni mtu aliyeogopewa sana.  Huyu  alikuwa
 ni wakala wa Chama tawala na Serikali. Moja ya majukumu yake ilikuwa ni
 kuwatambua, katika nyumba zake kumi, wale wote waliokuwa na mitazamo 
tofauti na ya Serikali na Mkuu wa Nchi. Ni wale walioitwa ’ Wapinga 
Maendeleo!’. Kuna waliosekwa rumande, kuna waliofungwa magerezani. 
Enzi
 zile viongozi watu wazima walisimama majukwaani na kusema; ” We have a 
One Party Democracy!” Katika dunia hii hakuna ‘ One Party Democracy’ 
bali ‘ One Party Dictatorship’. Hata kwenye nyumba mwanamme ukishaoa 
huwezi tena kutamka juu ya ‘ One Man Family!’- Na watoto wakiingia 
kwenye familia , nao pia wanatakiwa wawe na sauti.
Afrika
 Rais anategemea sana wasaidizi wake katika kuifanya kazi yake. Hivyo, 
mfumo dhaifu huzaa wasaidizi dhaifu pia. Mfano, pale Bungeni hakukuwa na
 haja yoyote ya mbunge kutolewa nje kwa kutamka ‘ JK ni Dhaifu’.   
Badala yake, ilikuwa fursa kwa wasaidizi wa JK kujenga hoja za kubomoa hoja za mbunge huyo. 
Kumtoa
 Mbunge nje kumemsaidia zaidi kuwasilisha ujumbe wake na hata ukaaminiwa
 na wengi. Maana, swali la hata wasiofutilia vipindi vya Bunge ni ‘ 
Kwani huyo Mnyika amesema nini?” Ni yale yale ya Zitto Kabwe kutolewa 
Bungeni kwa hoja ya Buzwagi. Nakumbuka kumsikia Mzee Malecela akisimama 
Bungeni na kutamka, kuwa dawa ya kidole chenye kansa ni kukikata!
Malecela
 na wengine katika CCM walisaidia, kwa kasi ya ajabu, kumtangaza na 
kumpa umaarufu Zitto Kabwe. Maana, wengi mitaani walitaka kukiona kidole
 hicho chenye kansa kinachokisumbua chama tawala na kikongwe hapa 
nchini, CCM.  
 Na
 mpaka hii leo, CCM wanarudia makosa yale yale ya jana. Na kwanini 
wanarudia? Ni kwa baadhi ya watendaji, kuingiwa hofu na wimbi hili la 
mabadiliko, hivyo kutojiamini na hata kufanya yale wanayodhani 
yatamfurahisha aliyewateua, kumbe, wanamharibia, na wanazidi kukipaka 
matope chapa chao.
Naam, tunaweza kuondokana na mfumo dhaifu kupitia Katiba mpya ijayo. Inawezekana.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0788 111 765 
 
 
No comments:
Post a Comment