Wednesday, June 13, 2012

BIFU YA AY NA PRODUCER WAKE HERMY B YAFIKIA HAPA




 AY
 HERMY B

"Ningependa kujibu shutuma zilizoandikwa  kuhusu uhusiano wangu na swahiba wangu A.Y. Ningependa ifahamike kwamba mimi na A.Y  kwa kipindi cha miaka 4 tumefanya kazi za muziki kwa karibu pamoja na kazi nyingine za biashara.  Ni kawaida na inaeleweka kwamba mahali popote watu wanapofanya kazi pamoja kugongana katika mawazo au lugha ni jambo la kawaida, na ndio changamoto zenyewe. Si jambo la ajabu kama mimi na swahiba wangu A.Y. kupishana katika kazi.


Hivyo  nimeona ni lazima nijibu kwani nikiiacha bila kujibu madhara yake yatakuwa  mabaya.  Kwanza napenda ieleweke sijawahi kuwa msimamizi wa kazi za A.Y zaidi ya kuwa producer wa nyimbo zake tu. Kipindi chote hicho nimekua natumia utaalamu wangu kwenye kutengeneza tu muziki wake. Maswala mengine yoooote amekuwa akifanya mwenyewe tena bila msaidizi.



Pia bila A.Y na MwanaFA kunipa nafasi kutengeneza muziki wao nisingekua hapa nilipo. Nadhani inaeleweka mahali popote duniani kwamba kipaji ili kifahamike kwa watu lazima kipitie kwa mtu fulani au mkondo fulani. Si ajabu kama kipaji changu cha kuproduce muziki kimeweza kufahamika kwa kupitia kwa A.Y. Mimi sio mungu labda ningekua sehemu nyingine na mafanikio makubwa zaidi au machache zaidi,lakini nachojua rafiki yangu amenipa ngazi ya kufika huku nilipo sasa, sijawahi kuficha hilo na hata wao wenyewe wanajua na bado nashukuru kwa hilo.



A.Y hajawahi kuingia mkataba wa aina yoyote na kampuni ya BHits Music Group Limited wala mimi binafsi uliombana kufanya kazi na mimi na sio mtu mwingine yoyote. Nimetengeneza nyimbo zisizopungua 30 za A.Y, kwa ajili ya albamu yake katika kipindi cha mwaka 2008 mpaka 2011. Baadhi ya nyimbo hizo zimeshatoka na nyingine bado zipo zikisubiri uhitaji wake. Wote tulikua na lengo la kutengeneza muziki kwa wingi na kuuza kwenye soko zuri la muziki ili tufaidike kwa pamoja.



Muda wote muziki ulikua unatolewa na unafanya vizuri kwa radio na T.V na show zilikua zinafanyika na zote nilikua nazijua iwe ndani ya nchi au nje ya nchi hii  hata malipo nilikua nafahamu ni kiasi gani na sijawahi kufichwa na A.Y kuhusu hilo.



Kutoelewana  kwetu kibiashara ilikuwa mwezi February mwaka huu yakihusu malipo ya album hiyo. Baada ya hapo niliamua kufunga mdomo wangu na nisingesema chochote kwani haya yalikua yananihusu mimi na rafiki yangu tu. Nimeamua kuongea sasa kwani nahisi nimeshambuliwa kwa mara ya pili kuhusu makubaliano haya na mara ya kwanza niliamua kukaa kimya.


Kwanza nataka mfahamu Katika kipindi cha kutokea 2008 mpaka leo hii (miaka 4) kwa matumizi ya nyimbo hizo, ambazo amekwishafanyia show nje na ndani ya nchi na nyingine kumpatia nominations na tuzo tofauti, nilichowahi kulipwa hakitaweza kuzidi shilingi milioni tatu kwa malipo ya awamu tofauti kwa miaka minne.


Kilichotokea ni kwamba, mwaka huu mwanzoni kabisa, A.Y aliwasiliana na mimi akiwa na mipango ya kuzindua albamu yake. Na alitaka kuzinunua zile nyimbo kutoka kwangu akiwa na mpango mpya wa kuiuza albamu kwa mpango wake binafsi pasi na mimi. Nilishindwa kuelewa nini anakifanya hasa alipoomba alipie wimbo mmoja mmoja tena kwa bei ya msanii wa kawaida anaehangaika kutoka.

Niliamua kukubali kwamba ameamua kufanya hivyo na sina nguvu ya kumzuia basi nikajaribu kupata malipo halisi ya kazi yangu. Ubishi wangu ulikua kwamba msanii mdogo hawezi kulipa bei sawa ya kurekodi na msanii mkubwa, kwani hata malipo ya msanii mkubwa na mdogo baada ya kazi yoyote iwe ya matangazo ama show huwa hayafanani. Bei niliyotaja haikua millioni kumi, ni uongo mtupu na kwa wimbo mmoja niliomba nilipwe millioni 2.
Akakubali kwa bei hiyo ya Millioni 2 japo nilihisi hakuridhika kabisa. Nilimtumia mkataba wa makubaliano yetu ambayo kweli baadae aliona kwamba bei hiyo kwake ni kubwa sana hivyo hatukusaini makubaliano. Tulibadilishana meseji kwa simu kwa muda mrefu sana na niliona biashara hii itavunja urafiki wetu.
Nilifikiria sana kwamba nyimbo hizi nimekaa nazo toka 2008 bila kuingiza chochote na maisha yanaenda pia. Sikuona sababu ya kuharibu urafiki wetu wa muda mrefu kwa mabishano haya. Kwa Ujumbe wa simu nilimueleza A.Y anakaribishwa aje achukue nyimbo zoooooote anazohitaji kwa albamu yake BURE (bila malipo).Lakini nilimuomba anisamehe sitomix zile ambazo bado hazijamixiwa, ila ampatie producer mwingine amfanyie hiyo kazi.
Mpaka  hii makala A.Y hajaja kuchukua hizo nyimbo na ndio naelewa kua hayupo na BHits tena na wala taarifa zote hizo mbili hajawahi kunipatia. Huu ndio ukweli halisi.
Swala la mimi kuwa na wivu na kinyongo na mafanikio ya A.Y ni uongo na nashangaa umetoka wapi . Kama kulipwa kidogo, huku nikiona A.Y anaingiza fedha nyingi kwa muziki tunaotengeneza pamoja basi ningekua nimegombana nae toka mwaka 2009 labda
Narudia kwamba nilikua najua kila show yake inapofanywa na sikuwahi kujisikia vibaya. Nataka utambue pia nilikua na akili timamu wakati nafanya kazi na A.Y na muda wowote nilikua na uwezo wa kubadili mawazo na kutaka tuandike makubaliano kwa karatasi ila sikufanya hivyo na wala sijutii chochote kwa utaratibu wetu wa hatari wa kufanya kazi bila mkataba wa maandishi na ndio maana nipo radhi hata sasa kumpatia nyimbo hizo bure kama nlivomwambia hapo mwanzo 


Nina meseji zote na email za mazungumzo yetu ambazo nilihifadhi nikijua ipo siku nitaonekana mimi ndie mkorofi, hivyo nachokisema nina hakika nacho asilimia 100

Picha nyingine mbaya ulioichora ni kujaribu kuonyesha kuna kutopendana kati ya maproducer. Mimi Master Jay na Marco Chali ni marafiki wazuri tu na mpaka leo hii nikiwa na shida na nikamhitaji Marco Chali au Master Jay nitampigia simu bila aibu kwani hakuna ugomvi kati yetu. A.Y, Master Jay na Marco Chali pia ni marafiki wa siku nyingi na katika kipindi cha miaka minne akiwa Bhits kwa hiari yake na sio mkataba, A.Y amekuwa akienda MJ records anapojiskia na mara kadhaa mimi nimeenda na A.Y na mara kadhaa nimeenda peke yangu tena kwa ajili ya shughuli zangu binafsi.
Pia ufahamu katika kipindi hicho A.Y alikua akitumia muda mwingi MJ Records kuliko Bhits na hiyo yote ilikua ni mipango yake binafsi. A.Y hajawahi kuzuiwa kufanya kazi na mtu mwingine kwani ni msanii huru.
Ndugu yangu mimi ni mtu mpole nisiye na ugomvi na mtu hapa mjini. Nasikitika sana kwa jinsi kwenye makala yako ulivyojitahidi kuonyesha kwamba mimi na swahiba wangu tumejenga uadui. 

No comments: